WAKAZI wawili wa kijiji cha
Sirorisimba, wilayani Butiama mkoani Mara, wamejeruhiwa kwa kuchomwa mishale, wakati
wakigombea ardhi kati yao na wakazi wa kijiji cha Mikomariro wilayani Bunda.
Polisi mjini Bunda imethibitisha
tukio hilo na kuwataja watu hao kuwa ni Hamisi Nyamhanga (38), aliyechomwa
mshale mgongoni na Samson Wambura (36), aliyechomwa mshale mguuni, wote wakazi
wa kijiji cha Sirorisimba wilayani Butiama.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sirorisimba, Alexander Makire, aliliambia
matalynewz leo kwamba, tukio hilo lilitokea juzi asubuhi, baada ya wakazi wa kijiji cha
Mikomariro kuvamia shamba la mkazi wa kijiji cha Sirorisimba na kuanza kulima
kwa jembe la kukokotwa na ng’ombe.
Makire alisema baada ya
mwenye shamba hilo kuwaona watu hao, alikwenda kuwauliza, lakini badala yake
watu hao waliamua kupiga yowe na watu wakakusanyika na kutokea vurugu kubwa,
ambapo watu wawili walijeruhiwa kwa kuchomwa mishale.
Kwa mujibu wa polisi, ambao hawakutaka kutajwa majina yao, kutokana na vurugu hizo, walifika
eneo la tukio wakiwa na uongozi wa wilaya ya Bunda na kuwatia nguvuni watu
wawili.
Waliwataja waliokamatwa kuwa ni Tulubeth Tundula (32) na Juma
Mwita Werema au Magere Kisheri (45), wote wakazi wa kijiji cha Mikomariro na
kwamba wanashikiliwa katika kituo cha polisi Butiama.
Walisema mtu mmoja
aliyejeruhiwa, amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Mara mjini Musoma na hali
yake inaendelea vizuri na kwamba mwingine hali yake ni nzuri na yuko
nyumbani.
No comments:
Post a Comment