Wednesday, 20 August 2014

Sheria ya Ushirika yawabana vigogo



  • Madiwani wawili CCM waachia ngazi

SHERIA mpya ya Ushirika imeanza kuwang’oa wanasiasa na viongozi wa serikali, ambapo madiwani wawili wa CCM wameachia ngazi.
Madiwani hao, Rashid Namwatika (Mnyawa-Tandahimba) na Rashid Mtingala (Mchauru –Masasi), wametangaza kuachia nafasi hizo ili kuendelea na nyadhifa ndani ya Vyama vya Ushirika.
Sheria hiyo mpya namba 6 ya mwaka 2013, ambayo utekelezaji wake umeanza Januari, mwaka huu, inawataka viongozi wa ushirika wenye nyadhifa za kisiasa ama serikali, kuchagua nafasi moja ya kutumikia ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.
Mtingala ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Mtwara, Masasi na Nanyumbu (
MAMCU) huku Namwatika akiwa ni Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Tandahimba na Newala (TANECU).
Akizungumza na matalynewz jana, Namwatika alithibitisha kung’atuka katika udiwani na kueleza kuwa alishauriana na viongozi wa CCM na amepewa baraza zote.
Alisema haikuwa kazi ngumu kukubaliwa kuchukua uamuzi huo kwa kuwa CCM ni muumini wa ushirika na kwamba, ana imani uamuzi huo utaimarisha maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mtingala alisema maamuzi aliyochukua ni magumu kutokana na mchango wake kuhitajika na wananchi wa pande zote.
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa kuna viongozi wengine wa serikali na vyama vya siasa, ambao kwa sasa wanatafakari maamuzi ya kuchukua kutokana na kubanwa na sheria hiyo.

No comments:

Post a Comment