Wednesday, 20 August 2014

HUJUMA RISITI FEKI ZA EFD Uchunguzi washika kasi, watuhumiwa waachiwa


NA MWANDISHI WETU

SAKATA la Kampuni za Corporate Image Group 
(CI Group) na Checknorats, kutuhumiwa kuhujumu uchumi wa taifa, limechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara kucharuka wakitaka wahusika wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho.
Hata hivyo, Ofisa Utawala Msaidizi wa Checknorats, Jatin Borhara na Mkurugenzi wa CI Group, Fires Nassoro, waliokamatwa kuhusiana na tuhuma hizo, wameachiwa.
Watuhumiwa waliokuwa wakishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Salender Bridge jijini Dar es Salaam, waliachiwa baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa  huku maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiendelea kuzifuatilia kampuni hizo kwa karibu kwa lengo la kubaini harasa ambayo serikali imepata.
Habari zinaeleza kuwa, uchunguzi zaidi unaendelea, ambapo maofisa wa polisi walisafiri kwenda Mwanza, ambako kunadaiwa kuna mashine zingine zinazotoa risiti feki.
Kampuni ya Checknorats, iliyopewa jukumu la kusambaza mashine za kieletroniki, iliiuzia CI Group mashine ambayo inatoa risiti feki na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Kupitia mashine hizo, serikali imekuwa ikilipa mrejesho wa fedha kwa kampuni kubwa nchini kwa kodi ambayo haijakusanywa, hivyo kukwamisha utelekezaji wa miradi ya maendeleo kwa Watanzania.
Hujuma hizo zimekuwa zikifanywa kwa muda mrefu sasa, hadi wiki iliyopita serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ilipobaini na kuvamia ofisi za kampuni hizo.
Kubainika kwa hujuma hizo kulitokana na Kampuni za Vodacom, Tigo, Tanzania Breweries Ltd (TBL), Serengeti Breweries Ltd na Benki ya MNB, kudai gawio la mrejesho huo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 
Kampuni hizo zimekuwa zikifanya biashara ya mamilioni ya shilingi na CI Group, lakini risiti wanazopewa ni feki, hivyo kuikosesha serikali mapato.
Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameibuka na kupongeza hatua za kufichua uhujumu uchumi huo na kutaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika hao.
Hata hivyo, wamelalamikia hatua ya serikali kuchelewa kuwapandisha kizimbani kwa madai ya uchunguzi kuendelea, jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa watuhumiwa kujipanga kufanya hujuma zingine ili kuharibu ushahidi.
Wakizungumza na Uhuru jana, Nassoro Masoud, alisema wafanyabiashara wengi walikuwa wakigomea matumizi ya mashine hizo kutokana na kunusa harufu ya hujuma miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa.
Alisema wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakifanya hila na hujuma mbalimbali ili kuiibia serikali huku wale wadogo na wa kati wakiendelea kukamuliwa kila kukicha.
“Huu ni uhujumu uchumi wa wazi na unastahili adhabu kali. Tunapongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mwigulu (Naibu Waziri wa Fedha), lakini hawa watu ni lazima wapande kizimbani kwa sababu kuna mengi tunayafahamu ila yamejificha,” alisema Masoud kwa niaba ya wenzake.
Juzi, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, alisema kampuni hizo zimekuwa zikitumia mashine ambazo hazijaidhinishwa kwa lengo la kuhujumu.
Pia, alisema walishazuiwa kutumia mashine hizo, lakini walikimbilia Mahakama ya Kodi na kufanikiwa kuruhusiwa, jambo lililoifanya TRA kuendelea kuzichunguza.
Hata hivyo, alisema bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kiwango cha fedha ambazo serikali imepoteza kutokana na hujuma hizo na kuchukua hatua stahiki.

No comments:

Post a Comment