Wednesday, 20 August 2014
Ngono yanunuliwa kwa debe la mahindi
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, wamesema Kata ya Ifwenkenya imekuwa tishio kwa ugonjwa wa Ukimwi, kutokana na vitendo vya ngono kufanyika hadharani bila kificho.
Imeelezwa kua mabinti wanaofanya biashara hiyo ya ngono ndani ya kata hiyo, wamefikia hatua hivi sasa wakiona mteja hana fedha za kulipia ngono, huomba kulipwa hata debe moja la mahindi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo jana, madiwani hao walisema hali imekuwa mbaya ndani ya kata hiyo, hivyo ni vyema hatua za tahadhari, ikiwemo kugawa kondomu zichukuliwe.
Diwani wa kata ya Mbangala, Ibrahimu Sambule, alisema biashara ya ngono iliyoibuka na kushamiri ndani ya kata ya Ifwenkenya, ni hatari kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa ukimwi wilayani Chunya.
“Mabinti waliopo ndani ya kata ya Ifwenkenya, hivi sasa wamefikia hatua wanauza ngono hadi kwa ujira wa kulipwa debe moja la mahindi. Wanasema wamekwenda kufanya biashara na siyo kucheza. Kwa kweli hali ni mbaya ndani ya kata hiyo,” alisema Sambule.
Aliitaka Kamati ya Afya na ukimwi ya halmashauri hiyo, kuliangalia suala hilo kwa uzito unaostahili, kwani mbali ya kata hiyo ya Ifwenkenya, kata ya Mkwajuni nayo ipo hatarini.
Diwani wa Kata ya Ifyenkenya, Piusi Omboka, alisema zinahitajika jitihada za kutosha kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kugawa kondomu na kutoa elimu kwa vijana, jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya ya ukimwi kwa kuachana kabisa na biashara hiyo.
Omboka alisema vitendo vya kufanya ngono hadharani, vimekuwa vikifanyika bila aibu na biashara hiyo imetawala katika mioyo ya watu.
Alisema hali hiyo imesababisha hata wahudumu wa nyumba za kulala wageni nao kujiingiza kwenye biashara ya mapenzi na waajiri wao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya (DMO), Dk.Wedson Sichalwe, alisema kata za Ifwenkenya, Mkwajuni na Lupa, ndizo zimekuwa na uhitaji mkubwa wa kondomu, kuliko maeneo mengine wilayani humo.
Dk.Sichalwe alisema halmashauri ya wilaya kwa kushilikiana na asasi zisio za kiserikali, kuanzia Julai, mwaka 2013, waliweza kusambaza kondomu 5,445,000 ili kukabiliana na maambukizi mapya ya ukimwi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment