Tuesday, 19 August 2014

Sungungusu waendesha msako wa wauaji wa albino


  •  Washukiwa waanza kupigiwa kura ya siri
  •  Wauaji wa vikongwe wabuni staili mpya

WALINZI wa jadi, maarufu kwa jina la Sungusungu, katika kata ya Isaka wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameanzisha utaratibu wa upigaji kura za siri kwa ajili ya kuwafichua watu wanaojihusisha na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa wimbi la  mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe na albino mkoani hapa. Mauaji hayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na imani za kishirikina.
Uchunguzi wa matalynewz umebaini kuwa, umezuka mtindo mpya wa mauaji dhidi ya vikongwe, ambapo wauaji kabla ya kutekeleza dhamira yao, huwaandikia barua wanawake wanaokusudiwa kuuliwa ili wajiandae kwa kifo.
 Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika kijiji cha Mwashigina, kata ya Isaka wilayani Kahama, Mtemi wa Sungusungu kata ya Isaka, Machimu Ndalo, alisema kutokana na kukithiri kwa mauaji hayo, wameamua zipigwe kura za siri.
 Ndalo alisema wilaya ya Kahama inaongoza mkoani Shinyanga kwa mauaji ya vikongwe, ambapo kila mwezi kunaripotiwa matukio ya mauaji yasiyopungua matatu, hali ambayo inawatisha wanawake wengi na kuwafanya waishi kwa hofu kubwa.
“Wiki iliyopita tuliendesha upigaji kura za siri katika kijiji cha Mwakata, ambapo zaidi ya wanakijiji 700 walijitokeza kupiga kura. Baada ya kuchambuliwa na kufanyika uchunguzi wa kina, tutawasilisha majina yote ya waliotajwa kwa viongozi wa serikali ili wachukuliwe hatua,” alisema .
mlemavu wa ngozi(Albino)
 Kwa upande wake, Ofisa Tarafa ya Isagenhe wilayani Kahama,


Kadigi Reuben, aliwaomba wakazi wa kijiji cha Mwashigina kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kuhakikisha wanawataja walengwa  wanaojihusisha na vitendo hivyo bila ya kutanguliza chuki binafsi au kukomoana.
Naye Ofisa Mtendaji wa kata ya Isaka, Nicholaus Maya, alisema matukio ya mauaji katika kata yake katika siku za hivi karibuni yamechukua sura mpya kutokana na wauaji kuamua kuwatumia  barua wanawake na kuzibandika katika milango ya nyumba zao.
“Hali ya mauaji kwa sasa inatisha, maana wauaji wanatuma barua kwa mtu wanayetaka kumuua kabla hawajatekeleza lengo lao na tayari kuna vikongwe wawili, Milembe Ngussa (70), mkazi wa Isaka na Ngolo Sakumi (69), wa kitongoji cha Kalangala wameuawa kwa mtindo huo,”alisema.
Baadhi ya wanawake waliozungumza na waandishi wa habari wakati wa  upigaji wa kura za siri katika kijiji cha Mwashigini, waliiomba serikali kuyafanyia kazi majina yote yatakayokuwa yameongoza katika kura hizo.

No comments:

Post a Comment