Wednesday, 20 August 2014

Marubani hatiani kwa kuchezea simu


NEW DELHI, India
MAMLAKA ya Usimamizi wa Anga nchini India, imewasimamisha marubani wawili wa Shirika la Ndege la Jet Ariways, kwa uzembe uliosababisha kudondosha ndege.
Taarifa ya mamlaka hiyo, ilisema marubani hao ambao bado hawajatajwa majina, walisimamishwa wiki iliyopita baada ya kukaribia kudondosha ndege yenye abiria 280.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege hiyo ilikuwa ikitoka Mumbai, nchini hapa kwenda Brussels, Belgiji.
Ilieleza kuwa ikiwa angani, rubani wa ndege hiyo alikwenda kujipumzisha na kumuachia majukumu msaidizi wake.
Ilisema baada ya kukabidhiwa kazi ya kuiongoza, msaidizi huyo aliendelea kuchezea simu yake bila kufuatilia mawasiliano na maelekezo aliyokuwa akiyapata kutoka viwanja mbalimbali alivyopita.
"Wakati ndege ikikatiza Uturuki ilihama eneo ilikoelekezwa na kushuka chini kwa mita 1,500 na kuingia katika anga ambalo wakati huo liliruhusiwa kutumiwa na ndege nyingine.
"Rubani alipopewa maelekezo hakuyasikia kwa kuwa alikuwa akichezea simu yake ya mkononi hali iliyowalazimu maofisa usalama wa anga wa uwanja wa ndege wa Ankara, kutangaza hali ya hatari," ilisema.
Mwaka 2011, sekta ya usafiri wa anga ilitetereka baada ya kukumbwa na kashfa ya marubani wengi kutumia vyeti vya kughushi huku wakiwa hawana uwezo katika taaluma hiyo.

No comments:

Post a Comment