Tuesday, 19 August 2014

Serikali kusaidia urutubishaji wa vyakula


SERIKALI imejipanga kufanikisha mpango wa kitaifa wa urutubishaji vyakula na kusimamia usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa lengo la kulinda afya ya walaji.

Hayo yamesemwa na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA),

Gaudensia simwanza

Gaudensia Simwanza alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana.

Akifafanua, Gaudensia alisema TFDA imeandaa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula (Tanzania food, Drugs and Cosmetics Regulations 2012).

Alisema hatua nyingine ni kuandaa miongozo ya udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kuwajengea uwezo wasindikaji kutekeleza matakwa ya kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula.

Akifafanua,  Gaudensia alisema  upo mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa mafuta ya kula yaliyoongezwa virutubishi na mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa unga wa mahindi ulioongezwa virutubishi ili kulinda afya ya mlaji.

Katika hatua nyingine, Gaudensia alibainisha kuwa mwongozo wa usimamizi wa kanuni za uongezaji virutubishi na mwongozo wa ukaguzi wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi, umeainisha taratibu za kufuata katika udhibiti wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu.

Aidha alisisitiza kuwa utoaji wa mafunzo kwa wadau kuhusu uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyooongezwa virutubishi kama vile wataalamu kutoka katika viwanda, ni muhimu kwa vile vinavyoongeza virutubishi kwenye vyakula.

Alilitaja jukumu jingine  la TFDA kuwa ni kusambaza vitendea kazi vinavyotumika katika uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula na kusimamia utekelezaji wa kanuni za uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inafanya majaribio ya uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula katika Halmashauri sita za mikoa ya Iringa, Kilolo, Iringa Vijijini, Njombe, Arusha, Karatu, Meru na Monduli.

No comments:

Post a Comment