Wednesday, 20 August 2014

Kiongozi mwingine Uamsho kizimbani



NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Jumuia ya Uamsho Zanzibar, Sheikh Mselem Ali Mselem, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akituhumiwa kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya kigaidi.
Sheikh Mselem amekuwa ni miongoni mwa viongozi wa juu wa Jumuia hiyo waliofikishwa mahakamani hapo, baada ya hivi karibuni kupandishwa kizimbani
Sheikh Farid Hadi Ahmed na wengine 20 kwa tuhuma hizo.
Mselem na Sheikh Abdallah Said Ali au Madawa, walifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali, George Barasa, waliwasomea washitakiwa hao mashitaka matatu.
Katika shitaka la kwanza, Sheikh Mselem na Abdallah wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014, katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kutafuta watu wa kushiriki vitendo vya kigaidi.
Sheikh Mselem na Abdallah, pia wanadaiwa katika kipindi hicho, walikubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki vitendo vya ugaidi.
Mshitakiwa Sheikh Mselem anadaiwa katika kipindi hicho  aliwaingiza nchini Sadick na Farah ili kushiriki vitendo vya kigaidi.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo litajwe kesho.
Hakimu Augustina alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo na washitakiwa walirudishwa rumande.
Mpaka sasa tayari watuhumiwa 21, akiwemo kiongozi mwingine wa Jumuia hiyo, Sheikh Farid, wameshapandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa tuhuma za kuwaingiza watu nchini kutenda vitendo hivyo na kuhifadhi watu waliotenda ugaidi.

Kesi inayomkabili Sheikh Farid na wenzake imepangwa kutajwa mahakamani hapo kesho. 

No comments:

Post a Comment