KAMATI Kuu ya CCM, chini ya Rais Jakaya Kikwete, jana imekutana mjini hapa kujadili masuala mbalimbali huku kubwa likiwa ni Katiba Mpya.
Kikao hicho cha juu kabisa ndani ya CCM, kinafanyika wakati Bunge Maalumu la Katiba likiendelea huku kukiwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe.Rais Kikwete alifungua kikao hicho saa 9:45 alasiri, ambapo awali aliwasili katika viwanja vya White House akiwa mwenye furaha na kuwakaribisha wajumbe.
Kabla ya kuzungumza lolote, alimuuliza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, iwapo idadi ya wajumbe imetimia, ambapo alielezwa kuwa imetimia huku mjumbe mmoja, Jerry Silaa akishindwa kuhudhuria kutokana na kubanwa na majukumu mengine.
Kinana alisema wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni 33 huku wajumbe wote wa Kamati Kuu ya CCM wakiwa 34.
Silaa, ambaye ni Meya wa Manispaa ya Ilala, yuko Jijini Arusha akihudhuria mkutano.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Rais Kikwete alisema ni cha kawaida na watajadili masuala mbalimbali yanayohusu Chama na kuyatolea maamuzi sahihi.
ìTunakutana tena kwa mara nyingine baada ya kukutana mwezi Julai, lengo likiwa ni kujadili mambo mbalimbali ya Chama chetu,î alisema Rais Kikwete.
Nje ya ukumbi wa White House, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, alikutana na waandishi wa habari na kuelezea kukerwa na taarifa potofu zilizoripotiwa kuhusiana na kikao hicho.
ìNimesikitishwa mno na baadhi ya taarifa kwenye vyombo vya habari, ni za uongo na sijui kwanini mnaandika mambo ya mtaani badala ya yake yanayotoka ndani ya Chama. Kama mna jambo si vyema mkauliza kwa sababu nipo kwa ajili yenu na nipo tayari kuitika wito wakati wowote mnapotaka kufahamu kinachoendelea. Ni Uhuru peke yake ndio limeandika taarifa sahihi,î alisema Nape.
Pia alionya kuwa hatakuwa tayari kuona CCM ikihusishwa na taarifa za mitaani na kuzifanya kuwa rasmi na kwamba, tabia hiyo ikiendelea, wahusika watapigwa marufuku kuingia ndani ili waendelea kupata habari za barabarani.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa, kikao hicho cha Kamati Kuu ni mahsusi kwa ajili ya kujadili mchakato wa Katiba Mpya. Kikao hicho kilitanguliwa na kile cha Sekretarieti, ambacho kilifanyika juzi.
Kikao cha Sekretarieti kilichoongozwa na Kinana, kilijadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa na shughuli za Chama.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ilikutana mjini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, ilijadili mchakato wa Katiba Mpya na kuelezea kuridhishwa kwake na mchakato huo.
Pia iliagiza kuendelea kwa vikao vya maridhiano baina ya CCM na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa lengo la kufikiwa maridhiano.
Hata hivyo, kundi hilo limeendelea kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kwa madai ya kuonewa na limemuomba Rais Kikwete kusitisha bunge hilo, vinginevyo litahasisha wananchi kufanya maandamano makubwa.
No comments:
Post a Comment