Wednesday, 20 August 2014

IS wamchinja mwandishi wa habari


BAGHDAD, Irak
KIKUNDI cha wapiganaji wa IS kimetangaza kumchinja mwandishi wa habari, James Foley aliyetekwa mwaka 2012.
Foley alitekwa nchini Syria alikokuwa akiripoti mapigano kati ya serikali na waasi wa huko.
IS ilitoa mkanda wa video unaoonyesha mwandishi huyo akichinjwa katika eneo ambalo bado halijajulikana ndani ya Irak.
Kwa mujibu wa mkanda huo, Foley, raia wa Marekani alichinjwa kwa kisu kidogo baada ya kutoa hotuba fupi iliyolaani uvamizi wa kijeshi wa nchi yake.
James Foley akiwa amepiga magoti muda mfupi kabla ya kuchinjwa
Foley alisikika akisema anajuta kuzaliwa Marekani kwa kuwa ndio iliyosababisha achinjwe baada ya jeshi la anga kuwashambulia wapiganaji wa IS katika opersheni yake ya kukisambaratisha kikundi hicho.
Aliiomba serikali yake kuyaondoa majeshi hayo ili kuwanusuru mateka wa Kimarekani wanaotekwa na wapiganaji hao akiwemo mwandishi mwenzake wa habari, Steven Joel Sotloff, aliyetekwa mwaka jana.
Mbali na kuishutumu Marekani, Foley aliyekuwa akiliripotia shirika la GlobalPost, alimlaumu ndugu yake wa kuzaliwa John, ambaye ni mwanajeshi wa anga wa Marekani kuwa amesababisha kifo chake.
"Siku ambapo wanajeshi wenzako walipoanza mashambulizi ya anga ndipo nami nilipohukumiwa kuchinjwa," alisema katika hotuba yake hiyo.
Kutokana na tukio hilo, Marekani imesema Rais Barack Obama, atatoa tamko.
Aidha, ilisema maofisa wa Intelejensia watafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo waliohusika na kwamba endapo itabaini ukweli hatua kali zitachukuliwa.
Maofisa walio katika safu ya ulinzi wa Rais Obama ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema inaonekana Foley alilazimishwa kuzungumza maneno hayo katika hotuba yake.
Kikundi cha IS kinaendesha mapambano dhidi ya serikali ya Irak ambapo pia kinahusika na mapigano yanayoendelea nchini Syria.

No comments:

Post a Comment