Monday, 25 August 2014

Hollande alivunja baraza la mawaziri

Arnaud Montebourg (kulia) akiwa na Benoit Hamon

PARIS, Ufaransa
RAIS Francois Hollande ametangaza kulivunja baraza la mawaziri baada ya kuibuka msuguano miongoni mwa mawaziri.
Aidha, amemtaka  Waziri Mkuu Manuel Valls aliyetangaza kujiuzulu, kuunda baraza jipya kabla hajaondoka kwenye kiti hicho.
Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya Ikulu Ufaransa vilisema kuvunjwa kwa baraza hilo kunatokana na kutofautiana kimtazamo kwa mawaziri kuhusu uchumi wa nchi.
Rais Hollande alimtaka Valls kuunda baraza jipya kabla ya kuondoka katika nafasi yake jambo ambalo linatafsiriwa kuwa huenda viongozi hao walikubaliana kuhusu uamuzi huo.
Mapema jana Valls alitangaza kujiuzulu wadhifa wa waziri mkuu kutokana na kile alichosema ni shutuma za baadhi ya mawaziri ndani ya baraza hilo dhidi ya sera ya uchumi.
Valls alimshutumu Waziri wa Uchumi, Arnaud Montebourg kwa kuikosoa serikali hadhari licha ya yeye mwenyewe kuwa sehemu ya watekelezaji wa sera hiyo.
Mbali na waziri huyo mwingine anayetoa upinzani dhidi ya serikali katika baraza hilo ni Waziri wa Elimu, Benoit Hamon ambao kwa pamoja wanatarajia kuachwa katika uteuzi mpya.
Hammon amekuwa akiishutumu Ufaransa kwa kufuata sera za uchumi zinazopangwa na Ujerumani jambo alililosema halitasaidia maendeleo ya taifa.

China yamuonya Papa Francis


VATICAN CITY, Vatican
CHINA imejibu kwa uangalifu mkubwa maombi ya Papa Francis ya kuanzisha mjadala mpya wa wazi na nchi hiyo, huku baadhi ya maofisa wa serikali wakiionya Vatican kuacha kuingilia dini ya nchi hiyo.
Akiwa njiani kurudi nyumbani baada ya ziara ya siku tano Korea Kusini, Papa Francis alisema yuko tayari kwenda China ìKwa hakika Hata kesho!î baada ya kupokea majibu mazuri ya salamu za nia njema kupitia telegramu mbili alizomtumia Rais Xi Jinping wakati akikatiza anga la China.
ìTunawaheshimu watu wa China,î Francis aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege yake Agosti 18. ìKanisa linachotaka ni uhuru wa majukumu yake katika kazi yake.î
Hiyo bado ni changamoto kubwa, kwa kuwa Vatican haina uhusiano wa kidiplomasia na China tangu mwaka 1951.
Kanisa Katoliki nchini China limegawanyika kati ya ëKanisa rasmií linalojulikana kama Chama cha Kizalendo cha Kikatoliki (CPA), linalowajibika kwa Chama cha Kikomunisti na Kanisa la chinichini ambalo linawajibika kwa Roma.
CPA linalosimamiwa na serikali ndilo lililoharakisha kujibu maombi ya Papa ya kuwa na mjadala mkubwa, ingawa kwa hadhari kubwa.
ìChina siku zote inalinda mamlaka yake na haki zake za kimsingi na kamwe haitaruhusu nguvu za kigeni kuingilia dini yake. Vatican inapaswa kuheshimu China katika masuala ya kidini,î
Makamu wa Rais wa CPA, Liu Yuanlong aliliambia gazeti la serikali la Global Times katika taarifa ambayo pia ilichapishwa kwa Kiingereza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China haifurahishwi na hatua ya Vatican kuitambua Taiwan, wakati Vatican nayo haifurahishwi na udhibiti wa China juu ya taasisi za kidini, hususan katika uteuzi wa maaskofu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Dini za Kidunia katika Chuo cha Sayansi Jamii cha China, Zhuo Xinping,  aliliambia gazeti lingine la serikali la  China Daily, kwamba anakaribisha hatua hiyo ya Papa, akisema amekuwa mstari wa mbele kuboresha ushirikiano wa Vatican na China tangU alipochaguliwa katika nafasi hiyo Machi mwaka jana.
Zhuo alimwelezea kiongozi huyo wa kiroho mwenye umri wa miaka 77 kutoka Argentina kama ìrafiki wa uchumi unaoendeleaî mwenye ìhisia maalumuî kwa watu wa nchi hizo pamoja na kuwa na asili ya Marekani Kusini.

Friday, 22 August 2014

MASANJA AWABOMOA WEMA , DIAMOND


COMEDIAN mwenye kofia ya uchungaji kwa sasa ,
Emmanuel Mgaya ‘ Masanja Mkandamizaji ’ hivi
karibuni aliwabomoa mastaa wapenzi Nasibu Abdul
‘ Diamond ’ na ubavu wake Wema Sepetu kwa
kuwaandikia waraka mzito unaohusiana na maisha
yao ya kila siku .
Komedian , Emmanuel Mgaya ‘Masanja
Mkandamizaji’.
Katika waraka huo , aliouweka kwenye ukurasa wake
wa Instagram, Masanja aliwataka wawili hao
kujirekebisha mapungufu yao kama kweli
wanapendana kwa dhati .
Akiuzungumzia waraka huo baada ya kuvutiwa
waya na kachala wa Ijumaa , Masanja alisema
hakuwa na nia mbaya kuwaandikia wapenzi hao
kama watu watakavyojaribu kufikiria , bali alifanya
hivyo kiroho safi na hivyo ni wajibu wao kuukubali
au kuukataa .
“Sina maana hiki nilichokisema lazima wakichukue
kama kilivyo, bali wao wenyewe wanapaswa
kuangalia mara mbilimbili ushauri wangu kabla
mambo hayajaharibika , ” alisema .
Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’
akipozi .
Alimtaka Wema kutambua kuwa mume ndiyo kichwa
cha nyumba , kwani kwa mujibu wa Diamond
inaonekana binti huyo hamsikilizi mwenziye.
“Naamini kabisa kwa mujibu wa muongozo
niliousoma kupitia maelezo ya Diamond kuwa
hamsikilizagi, hivyo anatakiwa kuomba msamaha
tena na tena , akubali kubadilika .”
WARAKA WENYEWE HUU HAPA
“Hili swala la Diamond na Wema nadhani Mungu
amemhurumia mmoja wapo kati ya hao wawili,
kama wangekuwa watu wa kuoana wangeshaoana
muda mrefu, uchumba gani mrefu kama wanasomea
udaktari? Rafiki yangu Nasibu kama kweli
mlipendana kwa dhati hizo kasoro zinarekebishika ,
maana hakuna mwanadamu aliye sahihi kwani hata
wewe Nasibu una mapungufu yako .
Staa wa filamu na mpenzi wa Nasibu Abdul
‘Diamond’, Wema Sepetu .
Na wewe dada yangu Wema lazima ujue mume
ndiyo kichwa cha nyumba kwa maelezo hayo
inaonyesha haumsikilizagi mwenzio , omba
msamaha kila mara na pia ukubali kubadilika .
Mi sipendi mkiwa mnaongozana wote kwenye shoo
ya usiku , mume anatakiwa aende kufanya kazi mke
abaki nyumbani akirudi mwili umepoa hata ujauzito
unaingia, sasa wote stejini mkirudi miili ya moto si
mtazaa popompo jamanii!!!

Thursday, 21 August 2014

JACKIE CHAIN ASEMA MWANAE ALIYEKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA CHINA AMEMUAIBISHA SANA


Kama mzazi, mwanao anapojihusisha katika kitendo
cha aibu ni lazima hata wewe mwenyewe utajiskia
aibu, ndivyo anavyojiskia muigizaji wa filamu za
Hollywood, Jackie Chan baada ya mtoto wake wa
kiume kukamatwa na dawa za kulevya.
Baba na mwana
Jacky Chan amesema mwanae aitwaye Jaycee
amemuaibisha sana yeye na familia nzima hasa
mama yake, baada ya kukamatwa na dawa za
kulevya nchini China.
Lakini Chain kama mzazi amemuahidi mwanae
kuwa atakuwa nae bega kwa bega licha ya kosa
alilolifanya. Pia kwa niaba ya Jaycee, ameiomba
radhi jamii kwa kitendo kilichofanywa na mtoto
mtoto wake ambacho hakileti picha nzuri kwa jamii.
Hii ndio barua aliyoiandika Jackie Chain na kuipost
kwenye website yake, baada ya taarifa za
kukamatwa kwa mtoto:
“When I first heard the news, I was absolutely
enraged”.
“As a public figure, I feel very ashamed; as his dad,
I’m very sad and disappointed. But the person who
feels heartbroken the most is his mom.”
“I hope our younger generation will learn from
Jaycee’s mistake and stay far away from drug
abuse.”
“I would like to take this opportunity and say to
Jaycee: you’ve done something wrong and you have
to be responsible for the consequences. I’m your
dad and I’ll always be with you. We will face the
road ahead of us together.”
“I should also take some of this responsibility
because as his dad, I didn’t teach him well.”
“Therefore, on behalf of Jaycee and myself, I extend
our deepest apologies to everyone for the negative
impact this has caused on society. Thank you.”

CHRIS BROWN NA KARRUECHE TRAN WATHIBITISHA KURUDIANA, CHRIS ANATAKA AMPATIE MTOTO?




Baada ya tetesi za hapa na pale juu ya kuachana
kwa mwimbaji wa R&B Chris Brown na girlfriend
wake Karrueche Tran na kurudiana, hatimaye Breezy
amethibitisha si tu wamerudiana bali anampenda na
anatakiwa aache mchezo.
Wote wawli kupitia akaunti zao za Instagram
wamethibitisha kurudiana kwao kwa kuweka post
tofauti.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram hiki ndicho
ameandika Breezy:
“@karrueche damn near 5 years and this woman still
putting up with my shit. Need to have this baby and
stop playing! Lol! My WCW”.
Kitu strange katika ujumbe wa Breezy ni, kumbe
wanakaribia miaka 5 kwenye uhusiano na
Karrueche?
February 8, 2009 ndio siku ambapo Chris Brown
alimpiga Rihanna ambaye alikuwa girlfriend wake na
kumsababishia majeraha usoni, na kwa hesababu za
haraka haraka miaka mitano anayoizungumzia
wanakaribia kuifikisha akiwa na Karrueche ni
kuanzia 2009.
Chris Brown na Riri walianza kudate 2008, licha ya
kufahamiana na kuanza urafiki toka 2005, Kwa
mujibu wa Wikipedia. Japo toka aanze kujihusisha
na Tran alikuwa akiwabadilisha mara kwa mara
Karrueche na Riri.
Siku moja iliyopita Karrueche naye alipost picha
(hapo chini) ya Breezy wakiwa kwenye dinner date:
Katika post nyingine ya Agosti 19, Karuche aliweka
picha yao na kuandika:
“Lovers.. Friends.. We love, we laugh, we fight.. It’s
complicated and I can’t explain it but it’s not for
you to understand but us .. My MCM”
So hapo kwenye “It’s complicated”, pana
‘summarize’ drama zote zinazoendelea katika
uhusiano wao, Asante Tran.

MADAWA YA KULEVYA DIAMOND KIMENUKA



NIkweli kimenuka ! Mbongo Fleva Nasibu Abdul
‘ Diamond Platnumz ’ yupo kikaangoni, habari zinadai
kwamba kila anaponyanyua miguu , kikosi cha
kupambana na kuzuia madawa ya kulevya nchini
chini ya kamishna wake, Godfrey Nzowa nao
wananyanyua miguu yao kumfuatilia, Amani
limesheheni.
Mbongo Fleva Nasibu Abdul ‘ Diamond Platnumz ’
akipozi .
Habari za kiintelijensia zilidai kwamba, kisa cha
kikosi hicho kufanya hivyo kinadaiwa kuwa , serikali
inamhofia kujihusisha na biashara hiyo haramu ya
kusafirisha madawa ya kulevya ‘ unga’ nje ya nchi
kwa kutumia kivuli cha kwenda kufanya shoo .
Akizungumza na wanahabari wetu jijini Dar ,
Jumatatu iliyopita , afisa mmoja wa ngazi ya juu wa
kitengo hicho ambaye hakupenda kuchorwa jina
gazetini, alisema Diamond amepewa maelekezo yote
muhimu.
MAELEKEZO ALIYOPEWA
“Tumempa maelekezo Diamond , atuletee mikataba
ya shoo zote anazokwenda kuzifanya nje ya nchi ili
tujiridhishe kama kweli ni halali au anakwenda kwa
ajili ya biashara nyingine .
“Hiyo yote inatokana na uchunguzi wetu kwake
kuhusu akaunti zake za benki kuonesha kwamba
ana fedha nyingi sana zinazotia shaka kama
amezipata kihalali , ” alisema afisa huyo.
‘Diamond Platnumz ’ akiwa kazini .
KUNUNUA NYUMBA
Afisa huyo aliendelea kusema kwamba, uchunguzi
wao pia umebaini kwamba, msanii huyo wa Bongo
amekuwa akinunua nyumba kila anaporejea kutoka
kwenye shoo zake nje ya nchi , jambo ambalo
taasisi haiamini kama kweli analipwa pesa nyingi
kwa shoo moja , kiasi cha kumwezesha kununua
nyumba jijini Dar .
“Tumebaini kwamba Diamond kila akirudi nchini
kutoka kwenye shoo zake hununua nyumba .
Analipwa kiasi gani cha fedha kule kwenye shoo?
Hapa ndipo tunaposimamia sisi, ” alisema afisa huyo
huku akigongea msumari kuwa Diamond mwenyewe
amekatazwa kuzungumza kwenye vyombo vya
habari kuhusu kutakiwa kuwasilisha mikataba ya
shoo zake za nje .
KUNA UKWELI?
Amani lilifuatilia na kubaini kwamba, Diamond
aliporejea kutoka kwenye safari yake ya Marekani
hivi karibuni , alinunua nyumba kwa Sh . milioni 80
iliyopo maeneo ya Mwananyamala - Magengeni, Dar .
Siku za nyuma , msanii huyo aliwahi kuripotiwa
kununua nyumba zaidi ya mbili maeneo ya
Kijitonyama, Dar , kiasi cha kuandikwa na vyombo
vya habari kwamba amenunua mtaa.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na
Madawa ya Kulevya Tanzania , Godfrey Nzowa.
KUHUSU AKAUNTI YA BENKI
Diamond mwenyewe aliwahi kuhojiwa katika Kipindi
cha Take- One kinachorushwa hewani na CloudsTV
ambapo alipoulizwa akaunti yake inasomaje, alijibu
kuwa ina zaidi ya bilioni moja hivi .
DONDOO ZA UWEZO WA DIAMOND
1. Ana utajiri unaozidi shilingi bilioni 1.
2. Yupo kwenye mazungumzo na promota wa
Rwanda kufanya shoo moja ya uwanjani ambayo
anaweza kulipwa dola 120 ,000 ( zaidi ya Sh . milioni
190) .
3. Malipo ambayo hupokea kwa shoo zake nyingi za
nje ya nchi hayashuki chini ya dola 25, 000 ( zaidi ya
Sh . milioni 40) .
4. Tangu mwaka 2011 mwishoni akaunti yake
haijawahi kushuka chini ya Sh . milioni 100.
5. Anamiliki nyumba kadhaa jijini Dar ambazo
amepangisha watu .
6. Ili kuvunja mkataba na aliyekuwa meneja wake ,
Papa Misifa ilibidi amlipe Sh . milioni 18.
NZOWA AZUNGUMZA NA AMANI
Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Kikosi cha
Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya
Tanzania , Nzowa ambapo alipopatikana na
kuulizwa, alisema :
Sehemu ya madawa ya kulevya yaliyowahi
kukamatwa.
“Ni kweli ! Sisi kila mtu mwenye kipato cha kutia
shaka lazima tumchunguze. Diamond kama ana
mali zote kwa nini tusimchunguze . Ikithibitika
anajihusisha na biashara haramu ya dawa za
kulevya ama zake ama zetu huo ndiyo utaratibu
wetu.”
DIAMOND SASA
Amani lilimsaka Diamond na kumuuliza kama
analijua kasheshe hilo ambapo alisema :
“Najua, ila nimegundua kuna watu wamepanga
kunishusha chini kisanii ndiyo wanaoeneza taarifa
kwamba mimi nasafirisha unga .”
Amani: Sasa unadhani kwa nini hao watu unaosema
wamependa kukushusha kisanii wasitumie njia
nyingine , hasa ya sanaa wakatumia hiyo ambayo
unasema si kweli ?
Diamond : We elewe hivyo kaka ( akakata simu) .
SAFARI ZA NJE
Kwa kipindi kirefu sasa Diamond ambaye ni mpenzi
wa Wema Isaac Sepetu , amekuwa akisafiri nchi
mbalimbali kwa shoo na mambo binafsi ambapo
mbali na nchi kibao za Bara la Afrika, ameshasafiri
nchi nyingi zikiwemo Marekani , Uingereza, China ,
Norway, Ujerumani , Dubai na nyinginezo .

Wednesday, 20 August 2014

Hali tete Gaza


GAZA CITY, Gaza
MAPIGANO yameanza upya katika eneo la Gaza baada ya kutulia kwa wiki moja.
Wapalestina 10 wameuawa hadi sasa wakiwemo mtoto na mke wa Kamanda wa jeshi la Hamas, Mohammed Deif.
Pande zote mbili zimeendelea kurusha makombora kwenye maeneo tofauti kulenga maadui ambapo kwa upande wa Hamas imesharusha makombora 70 tangu kuanza upya mapigano hayo usiku wa kuamkia jana.
Kuanza upya mapigano hayo kumevuruga mazungumzo ya amani yaliyokuwa yakiendelea nchini Misri ambapo Israel imetangaza kuwaondoa wajumbe wake wote waliokuwa wakishiriki.
Hamas imewarudisha wanajeshi wake 2,000 walioruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kukubaliana kusimamishwa kwa mapigano hayo wiki iliyopita.
Hadi sasa karibu Wapalestina 2,000 wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo Julai 8, mwaka huu wakati Israel ikipoteza watu 63.

Marubani hatiani kwa kuchezea simu


NEW DELHI, India
MAMLAKA ya Usimamizi wa Anga nchini India, imewasimamisha marubani wawili wa Shirika la Ndege la Jet Ariways, kwa uzembe uliosababisha kudondosha ndege.
Taarifa ya mamlaka hiyo, ilisema marubani hao ambao bado hawajatajwa majina, walisimamishwa wiki iliyopita baada ya kukaribia kudondosha ndege yenye abiria 280.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege hiyo ilikuwa ikitoka Mumbai, nchini hapa kwenda Brussels, Belgiji.
Ilieleza kuwa ikiwa angani, rubani wa ndege hiyo alikwenda kujipumzisha na kumuachia majukumu msaidizi wake.
Ilisema baada ya kukabidhiwa kazi ya kuiongoza, msaidizi huyo aliendelea kuchezea simu yake bila kufuatilia mawasiliano na maelekezo aliyokuwa akiyapata kutoka viwanja mbalimbali alivyopita.
"Wakati ndege ikikatiza Uturuki ilihama eneo ilikoelekezwa na kushuka chini kwa mita 1,500 na kuingia katika anga ambalo wakati huo liliruhusiwa kutumiwa na ndege nyingine.
"Rubani alipopewa maelekezo hakuyasikia kwa kuwa alikuwa akichezea simu yake ya mkononi hali iliyowalazimu maofisa usalama wa anga wa uwanja wa ndege wa Ankara, kutangaza hali ya hatari," ilisema.
Mwaka 2011, sekta ya usafiri wa anga ilitetereka baada ya kukumbwa na kashfa ya marubani wengi kutumia vyeti vya kughushi huku wakiwa hawana uwezo katika taaluma hiyo.

Ebola kufungia watu usiku


MONROVIA, Liberia
SERIKALI ya Liberia imepiga marufuku matembezi ya usiku ikiwa ni moja ya hatua za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola.
RAIS Ellen johson
Akitangaza msimamo huo wa serikali kupitia redio ya taifa,Rais Ellen Johnson Sirleaf, alisema hakuna yeyote atakayeruhusiwa kutoka nje kati ya saa 3.00 usiku hadi saa 6.00 asubuhi.
Waziri huyo alisema hatua hiyo inahusisha pia udhibiti wa mwingiliano wa ndani kati ya hapa na miji ya jirani.
Kwa mujibu wa waziri huyo, kuanzia muda huo vikosi maalumu vitasambazwa mitaani kusimamia utekelezaji wa amri hiyo na kwamba yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya jeshi kuamuru kupigwa risasi kwa mtu yeyote atakayeingia Liberia kwa nguvu.
Katika amri hiyo, jeshi lilisema hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia wala kutoka nje ya hapa hadi pale itakapotangazwa tofauti.
Hivi karibuni Shirika la Afya Dunia (WHO) lilitangza kuanza kusambaza msaada wa chakula kwa watu milioni moja walio kwenye eneo lililotengwa kutokana na hofu ya kusambaa Ebola.
WHO ilitangaza kusambaza msaada huo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kuwasaidia waathirika.

IS wamchinja mwandishi wa habari


BAGHDAD, Irak
KIKUNDI cha wapiganaji wa IS kimetangaza kumchinja mwandishi wa habari, James Foley aliyetekwa mwaka 2012.
Foley alitekwa nchini Syria alikokuwa akiripoti mapigano kati ya serikali na waasi wa huko.
IS ilitoa mkanda wa video unaoonyesha mwandishi huyo akichinjwa katika eneo ambalo bado halijajulikana ndani ya Irak.
Kwa mujibu wa mkanda huo, Foley, raia wa Marekani alichinjwa kwa kisu kidogo baada ya kutoa hotuba fupi iliyolaani uvamizi wa kijeshi wa nchi yake.
James Foley akiwa amepiga magoti muda mfupi kabla ya kuchinjwa
Foley alisikika akisema anajuta kuzaliwa Marekani kwa kuwa ndio iliyosababisha achinjwe baada ya jeshi la anga kuwashambulia wapiganaji wa IS katika opersheni yake ya kukisambaratisha kikundi hicho.
Aliiomba serikali yake kuyaondoa majeshi hayo ili kuwanusuru mateka wa Kimarekani wanaotekwa na wapiganaji hao akiwemo mwandishi mwenzake wa habari, Steven Joel Sotloff, aliyetekwa mwaka jana.
Mbali na kuishutumu Marekani, Foley aliyekuwa akiliripotia shirika la GlobalPost, alimlaumu ndugu yake wa kuzaliwa John, ambaye ni mwanajeshi wa anga wa Marekani kuwa amesababisha kifo chake.
"Siku ambapo wanajeshi wenzako walipoanza mashambulizi ya anga ndipo nami nilipohukumiwa kuchinjwa," alisema katika hotuba yake hiyo.
Kutokana na tukio hilo, Marekani imesema Rais Barack Obama, atatoa tamko.
Aidha, ilisema maofisa wa Intelejensia watafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo waliohusika na kwamba endapo itabaini ukweli hatua kali zitachukuliwa.
Maofisa walio katika safu ya ulinzi wa Rais Obama ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema inaonekana Foley alilazimishwa kuzungumza maneno hayo katika hotuba yake.
Kikundi cha IS kinaendesha mapambano dhidi ya serikali ya Irak ambapo pia kinahusika na mapigano yanayoendelea nchini Syria.

Ngono yanunuliwa kwa debe la mahindi


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, wamesema Kata ya Ifwenkenya imekuwa tishio kwa ugonjwa wa Ukimwi, kutokana na vitendo vya ngono kufanyika hadharani bila kificho.
Imeelezwa kua mabinti wanaofanya biashara hiyo ya ngono ndani ya kata hiyo, wamefikia hatua hivi sasa wakiona mteja hana fedha za kulipia ngono, huomba kulipwa hata debe moja la mahindi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo jana, madiwani hao walisema hali imekuwa mbaya ndani ya kata hiyo, hivyo ni vyema hatua za tahadhari, ikiwemo kugawa kondomu zichukuliwe.
Diwani wa kata ya Mbangala, Ibrahimu Sambule, alisema biashara ya ngono iliyoibuka na kushamiri ndani ya kata ya Ifwenkenya, ni hatari kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa ukimwi wilayani Chunya.
“Mabinti waliopo ndani ya kata ya Ifwenkenya, hivi sasa wamefikia hatua wanauza ngono hadi kwa ujira wa kulipwa debe moja la mahindi. Wanasema wamekwenda kufanya biashara na siyo kucheza. Kwa kweli hali ni mbaya ndani ya kata hiyo,” alisema Sambule.
Aliitaka Kamati ya Afya na ukimwi ya halmashauri hiyo,  kuliangalia suala hilo kwa uzito unaostahili, kwani mbali ya kata hiyo ya Ifwenkenya, kata ya Mkwajuni nayo ipo hatarini.
Diwani wa Kata ya Ifyenkenya, Piusi Omboka, alisema zinahitajika jitihada za kutosha kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kugawa kondomu na kutoa elimu kwa vijana, jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya ya ukimwi kwa kuachana kabisa na biashara hiyo.
Omboka alisema vitendo vya kufanya ngono hadharani, vimekuwa vikifanyika bila aibu na biashara hiyo imetawala katika mioyo ya watu.
Alisema hali hiyo imesababisha hata wahudumu wa nyumba za kulala wageni nao kujiingiza kwenye biashara ya mapenzi na waajiri wao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya (DMO), Dk.Wedson Sichalwe, alisema kata za Ifwenkenya, Mkwajuni na Lupa, ndizo zimekuwa na uhitaji mkubwa wa kondomu, kuliko maeneo mengine wilayani humo.
Dk.Sichalwe alisema halmashauri ya wilaya kwa kushilikiana na asasi zisio za kiserikali, kuanzia Julai, mwaka 2013, waliweza kusambaza kondomu 5,445,000 ili kukabiliana na  maambukizi mapya ya ukimwi.

Mangu awaangukia viongozi wa dini


Na mwandishi wetu
VIONGOZI wa dini wameaswa kuendelea kufanya ibada za kimwili na kiroho kwa waumini ili kuwajengea maadili mema.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya jamii na kupunguza matukio ya uhalifu na kwamba, viongozi hao wana nafasi kubwa ya kuhakikisha hilo linatekelezwa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu, alisema hayo jana wakati alipokutana na kuteta na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
shaaban bin simba
Mufti Shaaban Bin Simba. 

Mkutano huo uliowahusisha baadhi ya Masheikh wa mikoa nchini, Kadhi wa Zanzibar pamoja na Maimamu wa misikiti, ulifanyika jana kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi,  Oysterbay, Dar es Salaam. 
Alisema haijawahi kutokea duniani kwa polisi kula njama na viongozi wa dini katika kupambana na uhalifu na kuwataka kuongeza mahubiri kwenye nyumba za ibada ili jamii iweze kutenda mema.
Pia alisema kwa kupitia nyumba za ibada, jamii na viongozi waimarishe kamati za ulinzi ili kuhakikisha amani inakuwepo maeneo yote ya ibada.
Kwa upande wake, Mufti Simba alisema dini zote zinahimiza waumini kutenda mema na kujiepusha na vitendo viovu.
Amelitaka jeshi la polisi kuendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanaotenda uhalifu kwani, hata kwenye taasisi za dini nako kuna uhalifu.
Sheikh Mkuu wa mkoa wa Arusha, Shabani Juma, wakati akitoa salamu za mkoa huo, alisema hali kwa sasa ni shwari na amani, hivyo wana wajibu wa kulinda amani tuliyonayo.

Sheria ya Ushirika yawabana vigogo



  • Madiwani wawili CCM waachia ngazi

SHERIA mpya ya Ushirika imeanza kuwang’oa wanasiasa na viongozi wa serikali, ambapo madiwani wawili wa CCM wameachia ngazi.
Madiwani hao, Rashid Namwatika (Mnyawa-Tandahimba) na Rashid Mtingala (Mchauru –Masasi), wametangaza kuachia nafasi hizo ili kuendelea na nyadhifa ndani ya Vyama vya Ushirika.
Sheria hiyo mpya namba 6 ya mwaka 2013, ambayo utekelezaji wake umeanza Januari, mwaka huu, inawataka viongozi wa ushirika wenye nyadhifa za kisiasa ama serikali, kuchagua nafasi moja ya kutumikia ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.
Mtingala ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Mtwara, Masasi na Nanyumbu (
MAMCU) huku Namwatika akiwa ni Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Tandahimba na Newala (TANECU).
Akizungumza na matalynewz jana, Namwatika alithibitisha kung’atuka katika udiwani na kueleza kuwa alishauriana na viongozi wa CCM na amepewa baraza zote.
Alisema haikuwa kazi ngumu kukubaliwa kuchukua uamuzi huo kwa kuwa CCM ni muumini wa ushirika na kwamba, ana imani uamuzi huo utaimarisha maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mtingala alisema maamuzi aliyochukua ni magumu kutokana na mchango wake kuhitajika na wananchi wa pande zote.
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa kuna viongozi wengine wa serikali na vyama vya siasa, ambao kwa sasa wanatafakari maamuzi ya kuchukua kutokana na kubanwa na sheria hiyo.

Mbivu, mbichi Kamati Kuu ya CCM leo


KAMATI Kuu ya CCM, chini ya Rais Jakaya Kikwete, jana imekutana mjini hapa kujadili masuala mbalimbali huku kubwa likiwa ni Katiba Mpya.

Kikao hicho cha juu kabisa ndani ya CCM, kinafanyika wakati Bunge Maalumu la Katiba likiendelea huku kukiwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe.
Rais Kikwete alifungua kikao hicho saa 9:45 alasiri, ambapo awali aliwasili katika viwanja vya White House akiwa mwenye furaha na kuwakaribisha wajumbe.
Kabla ya kuzungumza lolote, alimuuliza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, iwapo idadi ya wajumbe imetimia, ambapo alielezwa kuwa imetimia huku mjumbe mmoja, Jerry Silaa akishindwa kuhudhuria kutokana na kubanwa na majukumu mengine.
Kinana alisema wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni 33 huku wajumbe wote wa Kamati Kuu ya CCM wakiwa 34.
Silaa, ambaye ni Meya wa Manispaa ya Ilala, yuko Jijini Arusha akihudhuria mkutano.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Rais Kikwete alisema ni cha kawaida na watajadili masuala mbalimbali yanayohusu Chama na kuyatolea maamuzi sahihi.
ìTunakutana tena kwa mara nyingine baada ya kukutana mwezi Julai, lengo likiwa ni kujadili mambo mbalimbali ya Chama chetu,î alisema Rais Kikwete.
Nje ya ukumbi wa White House, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, alikutana na waandishi wa habari na kuelezea kukerwa na taarifa potofu zilizoripotiwa kuhusiana na kikao hicho.
ìNimesikitishwa mno na baadhi ya taarifa kwenye vyombo vya habari, ni za uongo na sijui kwanini mnaandika mambo ya mtaani badala ya yake yanayotoka ndani ya Chama. Kama mna jambo si vyema mkauliza kwa sababu nipo kwa ajili yenu na nipo tayari kuitika wito wakati wowote mnapotaka kufahamu kinachoendelea. Ni Uhuru peke yake ndio limeandika taarifa sahihi,î alisema Nape.
Pia alionya kuwa hatakuwa tayari kuona CCM ikihusishwa na taarifa za mitaani na kuzifanya kuwa rasmi na kwamba, tabia hiyo ikiendelea, wahusika watapigwa marufuku kuingia ndani ili waendelea kupata habari za barabarani.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa, kikao hicho cha Kamati Kuu ni mahsusi kwa ajili ya kujadili mchakato wa Katiba Mpya. Kikao hicho kilitanguliwa na kile cha Sekretarieti, ambacho kilifanyika juzi.
Kikao cha Sekretarieti kilichoongozwa na Kinana, kilijadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa na shughuli za Chama.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ilikutana mjini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, ilijadili mchakato wa Katiba Mpya na kuelezea kuridhishwa kwake na mchakato huo.
Pia iliagiza kuendelea kwa vikao vya maridhiano baina ya CCM na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa lengo la kufikiwa maridhiano.
Hata hivyo, kundi hilo limeendelea kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kwa madai ya kuonewa na limemuomba Rais Kikwete kusitisha bunge hilo, vinginevyo litahasisha wananchi kufanya maandamano makubwa.

HUJUMA RISITI FEKI ZA EFD Uchunguzi washika kasi, watuhumiwa waachiwa


NA MWANDISHI WETU

SAKATA la Kampuni za Corporate Image Group 
(CI Group) na Checknorats, kutuhumiwa kuhujumu uchumi wa taifa, limechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara kucharuka wakitaka wahusika wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho.
Hata hivyo, Ofisa Utawala Msaidizi wa Checknorats, Jatin Borhara na Mkurugenzi wa CI Group, Fires Nassoro, waliokamatwa kuhusiana na tuhuma hizo, wameachiwa.
Watuhumiwa waliokuwa wakishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Salender Bridge jijini Dar es Salaam, waliachiwa baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa  huku maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiendelea kuzifuatilia kampuni hizo kwa karibu kwa lengo la kubaini harasa ambayo serikali imepata.
Habari zinaeleza kuwa, uchunguzi zaidi unaendelea, ambapo maofisa wa polisi walisafiri kwenda Mwanza, ambako kunadaiwa kuna mashine zingine zinazotoa risiti feki.
Kampuni ya Checknorats, iliyopewa jukumu la kusambaza mashine za kieletroniki, iliiuzia CI Group mashine ambayo inatoa risiti feki na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Kupitia mashine hizo, serikali imekuwa ikilipa mrejesho wa fedha kwa kampuni kubwa nchini kwa kodi ambayo haijakusanywa, hivyo kukwamisha utelekezaji wa miradi ya maendeleo kwa Watanzania.
Hujuma hizo zimekuwa zikifanywa kwa muda mrefu sasa, hadi wiki iliyopita serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ilipobaini na kuvamia ofisi za kampuni hizo.
Kubainika kwa hujuma hizo kulitokana na Kampuni za Vodacom, Tigo, Tanzania Breweries Ltd (TBL), Serengeti Breweries Ltd na Benki ya MNB, kudai gawio la mrejesho huo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 
Kampuni hizo zimekuwa zikifanya biashara ya mamilioni ya shilingi na CI Group, lakini risiti wanazopewa ni feki, hivyo kuikosesha serikali mapato.
Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameibuka na kupongeza hatua za kufichua uhujumu uchumi huo na kutaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika hao.
Hata hivyo, wamelalamikia hatua ya serikali kuchelewa kuwapandisha kizimbani kwa madai ya uchunguzi kuendelea, jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa watuhumiwa kujipanga kufanya hujuma zingine ili kuharibu ushahidi.
Wakizungumza na Uhuru jana, Nassoro Masoud, alisema wafanyabiashara wengi walikuwa wakigomea matumizi ya mashine hizo kutokana na kunusa harufu ya hujuma miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa.
Alisema wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakifanya hila na hujuma mbalimbali ili kuiibia serikali huku wale wadogo na wa kati wakiendelea kukamuliwa kila kukicha.
“Huu ni uhujumu uchumi wa wazi na unastahili adhabu kali. Tunapongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mwigulu (Naibu Waziri wa Fedha), lakini hawa watu ni lazima wapande kizimbani kwa sababu kuna mengi tunayafahamu ila yamejificha,” alisema Masoud kwa niaba ya wenzake.
Juzi, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, alisema kampuni hizo zimekuwa zikitumia mashine ambazo hazijaidhinishwa kwa lengo la kuhujumu.
Pia, alisema walishazuiwa kutumia mashine hizo, lakini walikimbilia Mahakama ya Kodi na kufanikiwa kuruhusiwa, jambo lililoifanya TRA kuendelea kuzichunguza.
Hata hivyo, alisema bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kiwango cha fedha ambazo serikali imepoteza kutokana na hujuma hizo na kuchukua hatua stahiki.

Kiongozi mwingine Uamsho kizimbani



NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Jumuia ya Uamsho Zanzibar, Sheikh Mselem Ali Mselem, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akituhumiwa kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya kigaidi.
Sheikh Mselem amekuwa ni miongoni mwa viongozi wa juu wa Jumuia hiyo waliofikishwa mahakamani hapo, baada ya hivi karibuni kupandishwa kizimbani
Sheikh Farid Hadi Ahmed na wengine 20 kwa tuhuma hizo.
Mselem na Sheikh Abdallah Said Ali au Madawa, walifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali, George Barasa, waliwasomea washitakiwa hao mashitaka matatu.
Katika shitaka la kwanza, Sheikh Mselem na Abdallah wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014, katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kutafuta watu wa kushiriki vitendo vya kigaidi.
Sheikh Mselem na Abdallah, pia wanadaiwa katika kipindi hicho, walikubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki vitendo vya ugaidi.
Mshitakiwa Sheikh Mselem anadaiwa katika kipindi hicho  aliwaingiza nchini Sadick na Farah ili kushiriki vitendo vya kigaidi.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo litajwe kesho.
Hakimu Augustina alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo na washitakiwa walirudishwa rumande.
Mpaka sasa tayari watuhumiwa 21, akiwemo kiongozi mwingine wa Jumuia hiyo, Sheikh Farid, wameshapandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa tuhuma za kuwaingiza watu nchini kutenda vitendo hivyo na kuhifadhi watu waliotenda ugaidi.

Kesi inayomkabili Sheikh Farid na wenzake imepangwa kutajwa mahakamani hapo kesho. 

Tuesday, 19 August 2014

Diwani Malembeka awapiga 'jeki' wanawake wajasiriamali


WANACHAMA wajasiriamali wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), jimbo la Ukonga, wametakiwa kuwa wabunifu wa kukuza mitaji wanayopatiwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za  ujasiriamali.

Diwani wa Kata ya Msongola, Angela Malembeka, alitoa mwito huo juzi katika mkutano wa makatibu wa UWT uliofanyika Kata ya Ukonga, Dar es Salaam.
Angela pia alikabidhi msaada wa sh. milioni nne kwa wanawake wajasiriamali wa kata nane za jimbo hilo, ambapo kila kata imepatiwa sh. laki 500,000. 
Kata zilizopatiwa fedha hizo ni Msongola, Ukonga, Chanika, Pugu, Majohe, Gongo la Mboto, Kitunda na Kivule
Angela alisema kiasi hicho cha fedha alichokitoa kwa wanawake hao ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kuwawezesha wananchi wake, hususani wanawake.
Alisema awali, wajasiriamali hao walipatiwa mafunzo yakiwemo ya kutengeneza batiki, vikoi na chaki, lakini tatizo lilikuwa katika kupata mitaji ya kufanya shughuli walizosomea kwenye kozi mbalimbali za ujasiriamali.
Licha ya changamoto zinazowakabili wanawake hao, ikiwemo ya kukosa mitaji ya uhakika, Angela alisema wanakabiliwa na changamoto ya masoko ya kudumu ya kuuzia bidhaa zao, hivyo alizitaka mamlaka zinazohusika kuwasaidia kupata soko.

Serikali kusaidia urutubishaji wa vyakula


SERIKALI imejipanga kufanikisha mpango wa kitaifa wa urutubishaji vyakula na kusimamia usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa lengo la kulinda afya ya walaji.

Hayo yamesemwa na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA),

Gaudensia simwanza

Gaudensia Simwanza alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana.

Akifafanua, Gaudensia alisema TFDA imeandaa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula (Tanzania food, Drugs and Cosmetics Regulations 2012).

Alisema hatua nyingine ni kuandaa miongozo ya udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kuwajengea uwezo wasindikaji kutekeleza matakwa ya kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula.

Akifafanua,  Gaudensia alisema  upo mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa mafuta ya kula yaliyoongezwa virutubishi na mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa unga wa mahindi ulioongezwa virutubishi ili kulinda afya ya mlaji.

Katika hatua nyingine, Gaudensia alibainisha kuwa mwongozo wa usimamizi wa kanuni za uongezaji virutubishi na mwongozo wa ukaguzi wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi, umeainisha taratibu za kufuata katika udhibiti wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu.

Aidha alisisitiza kuwa utoaji wa mafunzo kwa wadau kuhusu uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyooongezwa virutubishi kama vile wataalamu kutoka katika viwanda, ni muhimu kwa vile vinavyoongeza virutubishi kwenye vyakula.

Alilitaja jukumu jingine  la TFDA kuwa ni kusambaza vitendea kazi vinavyotumika katika uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula na kusimamia utekelezaji wa kanuni za uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inafanya majaribio ya uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula katika Halmashauri sita za mikoa ya Iringa, Kilolo, Iringa Vijijini, Njombe, Arusha, Karatu, Meru na Monduli.